Wallah bin Wallah alizaliwa mwakani 1952 kule Nyakach, wilaya ya Nyando[1]. Jina alilopewa na wazazi wake lilikuwa Ndedah lakini alilibadilisha baadaye maana aliliona kana kwamba lilikuwa likimsaliti kama mkabila. Alilichukua jina la babake Wallah na baadaye akaona ni vyema kujiita Wallah mwanawe Wallah. Hivyo, jina Wallah bin Wallah likakita mizizi. Wallah alisomea nchini Tanzania maana alifuatana na babake aliyekuwa akifanya kazi na kampuni ya reli ya Afrika Mashariki huko Tanzania. Alijiunga na shule ya msingi la Lukungu alikosomea kutoka darasa la kwanza hadi la nne. Baadaye alijiunga na shule ya Bukumbu alikosomea hadi darasa la saba na kuhitimu katika mtihani wa G.E.E.
Maisha ya Wallah shuleni hayakuwa mepesi maana babake hakuwa akimpa msaada na mara kwa mara, Wallah alijilipia karo. Alifanya hivi kwa kuchuuza samaki pamoja na kuwanyoa wenzake ili apate pesa. Baada ya shule ya msingi, alijiunga na shule ya seminari ya Nyegezi ambako alikuwa akisomea somo la dini ya Kikristo. Hakumaliza hayo masomo maana aling'amua kwamba kama angetaka kuendeleza ujuzi wa Kiswahili, alifaa awe Muislamu. Aliacha shule na kurudi Kenya alikojiunga na shule ya upili ya Ravals, Latema. Aliweza kupata diploma ya ualimu katika chuo cha Morogoro Teachers' College mwakani 1976.
Baada ya shule, Wallah alianza kazi ya ualimu wa Kiswahili. Akiendelea kufunza katika shule mbalimbali Kenya kama vile Misiani Girls, Moi Girls Isinya, aliweza kufanya shahada ya Kiswahili na Kiarabu. Baadaye, aliendeleza uchu wake wa kukikujua Kiswahili kwa kufanya Shahada ya Uzamili katika chuo cha Dar es Salaam